SHULE NNE ZANZIBAR ZANUFAIKA NA VIFAA VYA TEHAMA KUTOKA UCSAF

  • 31 August, 2023
SHULE NNE ZANZIBAR ZANUFAIKA NA VIFAA VYA TEHAMA KUTOKA UCSAF

Kupitia mradi wa kuunganisha shule na mtandao wa intaneti, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Zanzibar wamepeleka vifaa vya TEHAMA kwenye Skuli nne (4) za Sekondari Zanzibar pamoja na  kufanya ukarabati wa maabara za kompyuta na uwekaji wa miundombinu ya intaneti. Shule za sekondari zilizonufaika na mradi huu ni pamoja na, Kizimkazi Dimbani, Kizimkazi Shehia ya Mkunguni, John Pombe Magufuli na Hasnuu Makame.

Hadi sasa ukarabati wa maabara tatu za kompyuta na uwekaji wa miundombinu ya intaneti katika shule hizo umekwishafanyika katika shule za Sekondari Kizimkazi Dimbani, Kizimkazi Sekondari Shehia ya Mkunguni na John Pombe Magufuli Mjini Kati. Aidha pamoja na kufanya ukarabati wa maabara za kompyuta, uwekaji wa miundombinu wa vifaa vya TEHAMA katika shule hizo, uwekaji wa samani na viyoyozi kwa ajili ya matumizi tarajiwa umefanyika pia.

Jumla ya gharama kwa mahitaji hayo inakadiriwa kuwa TZS 315,423,160/- ambayo inahusisha uwekaji wa Marumaru na upakaji wa rangi kweye milango, uwekaji wa miundombinu ya umeme, taa, switch na sockets (Electrical Installations), ufungaji wa miundombinu ya TEHAMA, uwekaji wa miundombinu ya Mifumo hewa pamoja machine za kupooza hewa (Air Condition installations) na Ufungaji wa meza za kuwekea kompyuta na kufanyia kazi (Woodwork framing installations).

Jumla ya Kompyuta sitini zimekwishatolewa, projecta tatu, printa tatu, kamera sita pamoja na viti sitini. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa mradi wa kuunganisha shule (Schoool Connectivity Project) unatekelezwa katika shule zote za Serikali nchini katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.