Vituo vya TEHAMA kwa jamii kutengeneza ajira, Zanzibar

  • 15 April, 2023
Vituo vya TEHAMA kwa jamii kutengeneza ajira, Zanzibar

Jumla ya wakazi 3,708 Visiwani Zanzibar, wengi wao wakiwa vijana wamepata elimu ya kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano inayotolewa katika vituo vilivyojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) visiwani humo.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi( SMZ) Dkt Mzee Mndewa.

Amesema vituo hivyo vimejengwa kwa lengo la kupeleka elimu ya TEHAMA kwa wananchi ili kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa kidigitali kwa kutumia TEHAMA.

Amesema, ni muhimu kuwajengea uwezo ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidigitali. UCSAF imejenga vituo kumi na moja( 11) katika wilaya zote za Unguja na Pemba na kuvikabidhi kwa Wizara hiyo ili iweze kuvisimamia.

Vijana wenye uelewa wa TEHAMA hujitolea kufundisha wenzao elimu ambayo inaweza kuwasaidia kujiajiri kwa kufungua sehemu za kutoa huduma za kuprinti, kutoa photocopy, kutengeneza kadi za matukio mbalimbali kwa kutumia program za kompyuta kama vile Microsoft word, adobe na publisher.