Wanafunzi Msomera wanufaika na vifaa vya TEHAMA kutoka UCSAF

  • 22 September, 2023
Wanafunzi Msomera wanufaika na vifaa vya TEHAMA kutoka UCSAF

Shule ya Msingi Samia Suluhu Hassan iliyoko katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni Mkoani Tanga imenufaika na vifaa vya TEHAMA kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF). Vifaa hivyo vimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuunganisha shule za umma na mtandao wa intaneti pamoja na kuzipatia vifaa vya TEHAMA.

Jumla ya kompyuta za mezani ( desktop) 20, laptop moja, printa mbili na projecta moja zimetolewa kwa shule hiyo ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata nafasi ya kujufunza kwa kutumia vifaa vya TEHAMA kuanzia hatua za awali, ili kukuza ushindani na uelewa wa matumizi ya vifaa hivyo.

Shule hiyo yenye wanafunzi wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya kimasai ambao walihama kwa hiari kutoka Ngorongoro kuelekea katika kijiji cha Msomera, kijiji ambacho Serikali imefanya uboreshaji mkubwa wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mawasiliano.

Kompyuta hizo zimefungwa katika chumba maalum ( kompyuta Lab), ambapo wanafunzi huingia kwa awamu ili waweze kujifunza. Kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kompyuta zote zilizo katika maabara hiyo zimeunganishwa na mtandao wa intaneti.