Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu yaipongeza UCSAF

  • 18 March, 2022
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu yaipongeza UCSAF

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikiongozwa na mwenyekiti wake, Mhe. Selemani Kakoso, imefanya ziara ya kukagua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na kampuni ya simu ya Vodacom kwa ruzuku ambayo hutolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF). Mnara huo umejengwa katika kijiji cha Nyampande Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, unatoa huduma ya mawasiliano ya simu kwa wananchi takribani 600,000.

Katika ziara hiyo, Kamati iliambatana pia na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Nape Moses Nnauye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Mohammed Khamis Abdulla, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu ya Vodacom, Sitholizwe Mdlalose.

Kamati imeipongeza UCSAF kwa kuzingatia na kufanyia kazi maelekezo ambayo hutolewa na Kamati hiyo, kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma ya mawasiliano inafika kwa wananchi wa vijijini na maeneo ya pembezoni ambako huduma hiyo ni hafifu ama haipatikani kabisa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema, Mfuko unatekeleza miradi 40 katika Mkoa wa Mwanza pekee. Miradi 18 kati ya miradi hiyo imekamilika na mingine utekelezaji unaendelea.

Kwa upande wake Diwani ya Kata ya Nyampande, George Kazungu ameishukuru Serikali kwa kufikisha huduma hiyo muhimu katika Kata ya Nyampande, kwa kuwa awali wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu ili kufuata eneo lenye mtandao ili waweze kuwasiliana.