Rais Samia aagiza vibali vya ujenzi wa minara vitolewe haraka.

  • 24 May, 2023
Rais Samia aagiza vibali vya ujenzi wa minara vitolewe haraka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia Utiaji saini mikataba ya kupeleka huduma ya Mawasiliano vijijini, ambapo jumla ya minara 758 itajengwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Mikataba hiyo ni baina ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa upande wa Serikali pamoja na watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini ambao ni makapuni ya simu ya Vodacom, Tigo, Airtel, Halotel na TTCL.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia ameipongeza UCSAF kwa kutekeleza mradi huo mkubwa ambao utasaidia kutatua changamoto ya mawasiliano vijijini, kwa kuwa mara utakapokamilika watanzania wapatao milioni 8.5 watapata huduma ya mawasiliano.

Ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati, Mhe. Samia amezitaka taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali kuhakikisha kuwa, vibali vyote vinatolewa ndani ya mwezi mmoja. Kwa upande mwingine, ameiagiza UCSAF kushirikiana na TARURA ili kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara inafika katika maeneo yote ya mradi, lakini pia ameagiza Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inafikishwa katika maeneo yote ambayo minara hiyo itajengwa.

Katika utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) watajenga minara 104, Vodacom watajenga minara 190, Airtel watajenga minara 168, Tigo watajenga minara 262 na Haloteli watajenga minara 34.