Habari

Watanzania watakiwa kutumia mawasiliano katika kujiletea maendeleo
  • 15 Dec, 2021
Watanzania watakiwa kutumia mawasiliano katika kujiletea maendeleo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania kutumia mawasiliano katika kujiletea maendeleo pamoja na kupata maarifa muhimu mbalimbali ikiwemo taarifa za kilimo, ufugaji pamoja na biashara.
 
Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati akizindua mnara wa mawasiliano ya simu, uliojengwa na kampuni ya simu Tanzania (TTCL) kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika kata ya Kajana Kijiji cha Kasumo wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. 


Amesema serikali inaendelea kuboresha huduma za mawasiliano hasa maeneo ya mipakani ili kuharakisha maendeleo ya wananchi pamoja kuongeza ulinzi na usalama katika maeneo hayo.

Makamu wa Rais amesema uwepo wa huduma za intaneti hasa katika maeneo ya vijijini ni kichocheo kikubwa cha kuboresha huduma za kijamii pamoja na kufungua fursa za kiuchumi katika taifa.
 
Amewasihi wananchi wa Vijijini vilivyonufaika na mawasiliano hayo kuyatumia katika kujitengenezea ajira ikiwemo kuanzisha biashara bunifu zinazotokana na uwepo wa mawasiliano.
 
Aidha Dkt. Mpango amewataka wananchi wa Kasumo kutumia mawasiliano hayo kutoa taarifa muhimu zikiwemo za wahamiaji haramu, uhalifu pamoja na ajali za kimiundombinu kama ya umeme ili kusaidia serikali kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na changamoto hizo

Tanzania Census 2022