Karibu

Justina Mashiba photo
Bi. Justina Mashiba
Mtendaji Mkuu

: ceo@ucsaf.go.tz

: +255 26 2965771

Wapendwa watanzania wenzangu,

Ili Kufanikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano Tanzania kwa kikamilifu na kwa usawa, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unalenga kuimarisha uwezo wa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano nchini ili kuhakikisha ufikiaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo yote yenye mawasiliano hafifu pamoja na yale yasiyo na huduma hiyo kabisa.

Katika kutekeleza majukumu yake, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umejielekeza katika kubaini maeneo ya miradi ya mawasiliano ambayo yanaweza kupata ruzuku Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma za mawasiliano ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia katika uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla.

Tangu kuanza kazi kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) mwaka 2009, kumekuwa na mafanikio mengi katika sekta ya mawasiliano, miongoni mwa mafanikio ambayo UCSAF imeyapata mpaka sasa ni asilimia 66 ya maeneo ya kijeografia kupata huduma za mawasiliano, asilimia 96 ya wananchi wanaweza kupata mawasiliano pamoja na kuongeza matumizi ya intaneti ambapo Mfuko unatekeleza mradi wa kuiongezea uwezo minara iliyokuwa katika teknolojia ya 2G kwenda 3G.

Kwa upande wa kuboresha mawasiliano ya simu, Mfuko umekuwa ukishirikiana na watoa huduma za mawasiliano kwa kutoa ruzuku ambayo itawawezesha watoa huduma kufikisha huduma katika maeneo yasiyo na mawasiliano ama yenye mawasiliano hafifu.

Kumekuwepo pia na changamoto ya mawasiliano ya simu pamoja na usikivu wa radio katika maeneo mengi yaliyoko mipakani. Mfuko unatekeleza pia miradi mbalimbali ya kuboresha mawasiliano katika maeneo hayo kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Mwisho, UCSAF itaendelea kuratibu upatikanaji wa huduma za Mawasiliano vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano duni kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya Mawasiliano ili kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Nawatakia mafanikio mema,

Mtendaji Mkuu.