UCSAF YAKAMILISHA MRADI WA KUBORESHA UWEZO WA MINARA 304 KUTOKA 2G KWENDA 3G/4G.

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), umekamilisha utekelezaji wa mradi wa kuongeza uwezo wa minara (upgrade), minara 304 iliyokuwa imejengwa katika teknolojia ya kizazi cha pili pekee yaani 2G ili iweze kufikia teknolojia ya 3G na 4G kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma ya mtandao wa intaneti.
Utiaji saini wa mradi huu ulifanyika tarehe 13 Mei 2023 kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali, ambapo Serikali kupitia UCSAF iliingia makubaliano na watoa huduma (Makampuni ya simu) kuongeza uwezo wa minara hiyo kwa lengo ya kuhakikisha kuwa, wananchi katika maeneo yenye minara hiyo wanaanza kupata huduma za mtandao wa intaneti.
Faida zinazopatikana kutokana na kukamilika kwa mradi huo ni pamoja na wananchi kuweza kutumia mtandao wa intaneti kwenye simu zao pamoja na vifaa vingine vya kidijitali, kwa kuwa teknolijia ya 3G na 4G inaruhusu matumizi mbalimbali ya intaneti kama vile kufanya miamala ya kibenki, kuangalia video mtandaoni pamoja na kuiwezesha Serikali kuboresha huduma za kijamii kama vile kuwezesha mifumo ya malipo na huduma zingine zinazotolewa kwa wananchi.
Jumla ya makampuni ya simu manne yalipatiwa ruzuku na serikali kwa ajili ya kuongeza uwezo wa minara hiyo 304 ambapo kampuni ya simu ya Airtel ilikuwa na minara 32, Vodacom minara 69, Honora (tigo) minara 148 na TTCL minara 55.