MINARA 372 KATI YA 758 ILIYOPANGWA KUJENGWA IMEKAMILIKA: WAZIRI SILAA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.), amesema jumla ya minara 372 kati ya 758 iliyopangwa kujengwa imekamilika, kati ya hiyo minara 332 imewashwa na tayari imeanza kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Silaa ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge pamoja na utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2024/2025, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Waziri amesisitiza kuwa kukamilika kwa minara hiyo ni sehemu ya juhudi kubwa za serikali ya awamu ya sita kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, hususan katika maeneo ya vijijini ambako huduma za mtandao wa simu na intaneti zilikuwa hafifu.
Aidha, Waziri Silaa amefafanua kuwa minara 304 iliyokuwa imejengwa kwa teknolojia ya kizazi cha pili (2G) imeongezewa uwezo (upgrade), ambapo sasa minara hiyo ina uwezo wa kutoa huduma kwa teknolojia ya 3G na 4G. Hii ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za intaneti, kuongeza kasi ya mawasiliano kwa wananchi, na kuongeza matumizi ya intaneti hasa kwa kuzingatia umuhimu wa teknolojia katika maendeleo ya uchumi na jamii.
Jumla ya makampuni ya simu manne yalipatiwa ruzuku na serikali kwa ajili ya kuongeza uwezo wa minara hiyo 304 ambapo kampuni ya simu ya Airtel ilikuwa na minara 32, Vodacom minara 69, Honora (tigo) minara 148 na TTCL minara 55 na hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma za intaneti zenye ubora wa juu.
Serikali kupitia UCSAF inaendelea kuwekeza katika kujenga na kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha kuwa huduma za intaneti, simu, na teknolojia nyingine zinapatikana kwa wananchi wote bila kujali mahali walipo, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi.