BILIONI 6.5 KUBORESHA HUDUMA ZA MAWASILIANO VIJIJINI MKOANI SINGIDA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi, amepongeza mkoa wa Singida kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa minara 32 inayojengwa katika Mkoa huo kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.5 ikiwa ni sehemu ya minara 758 inayoendelea kujengwa nchini kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Mhandisi Mahundi ametoa pongezi Mkoani Singida, Machi 27, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Unyahati, Jimbo la Singida Mashariki.
Pamoja na pongezi hizo, Mhandisi Mahundi amewataka watoa huduma kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi wa minara 758 ili kukamilisha kwa wakati bila kuomba muda wa nyongeza kwani mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 44 na mwisho wa utekelezaji wake kwa mujibu wa mkataba ni Mei 12, 2025.
Alisisitiza kuwa jukumu kubwa la Wizara hiyo ni kuhakikisha kuwa adhma ya Tanzania ya Kidijitali inatimia kwa kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inajengwa kwa wakati, ili wananchi wote wafikiwe na huduma za mawasiliano.
Awali, akisoma taarifa ya hali ya mawasiliano kwa mkoa wa Singida, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati,Bw. Asajile Mwakisisile, alisema kuwa hadi kufikia Desemba 2024, Mkoa wa Singida una jumla ya minara 225 ya mawasiliano ya simu.
Naye Kaimu Meneja wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Kati, Shirikisho Mpunji, alisema kuwa kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, mkoa wa Singida umepata jumla ya minara 32 inayojengwa katika kata 31, huku vijiji 55 na wakaazi takribani 835,641 wakitarajiwa kunufaika.
Hadi kufikia Machi 2025, utekelezaji wa ujenzi wa minara katika kata 15 kati ya 32 ulikuwa umekamilika, na tayari wakazi wa maeneo hayo wananufaika na huduma za mawasiliano.