WALIMU 700 KUJENGEWA UWEZO WA MATUMIZI NA UTUNZAJI WA VIFAA VYA TEHAMA.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesisitiza umuhimu wa walimu kuwa na ujuzi wa kutumia na kutunza vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kuhakikisha vifaa vinavyotolewa katika shule vinatumika ipasavyo na kuchangia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati akifungua mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 700 wa shule za sekondari za umma nchini, yanayoratibiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Dar es salaam ( UDSM) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Mafunzo hayo yanalenga kuwapatia walimu mwongozo na ujuzi wa matumizi sahihi pamoja na utunzaji wa vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa na UCSAF katika shule husika, pamoja na shule zilizo kwenye mpango wa kufikishiwa vifaa hivyo. Kati ya walimu 700 wanaoshiriki, ambapo kati yao 100 ni walimu wenye mahitaji maalum ya kuona, hatua inayolenga kuhakikisha juhudi za kuongeza ujuzi wa kidijitali katika elimu zinazingatia ushirikishwaji na fursa sawa.
Mhe. Kairuki pia amesisitiza matumizi ya maabara mtandaoni (virtual laboratories) katika ufundishaji, hususan katika masomo ya sayansi, akieleza kuwa teknolojia hiyo itawapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo huku ikisaidia kupunguza gharama za matumizi ya kemikali na vifaa vya maabara. Aidha, amewataka walimu kuwaelimisha wanafunzi kuhusu matumizi salama, yenye uwajibikaji na maadili ya intaneti pamoja na akili bandia (Artificial Intelligence – AI).
Waziri amewataka walimu wanaoshiriki mafunzo hayo kuwashirikisha wenzao maarifa na ujuzi watakaopata baada ya kumaliza mafunzo, pamoja na kuhakikisha vifaa vya TEHAMA vinatunzwa na kutumiwa ipasavyo. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali kupitia UCSAF unatumika kikamilifu katika kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na kuongeza ujuzi wa kidijitali kwa wanafunzi.
#UCSAF #MawasilianoKwaWote #MafunzoYaTEHAMAKwaWalimu