UJENZI WA MINARA 758 YA MAWASILIANO WAFIKIA ASILIMIA 89.58

Mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu unaotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kwa kasi na kufikia hatua ya kuridhisha, ambapo hadi sasa jumla ya minara 679 kati ya 758 iliyopangwa tayari imekamilika. Hii ni sawa na asilimia 89.58 ya utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, hususan wakazi wa maeneo ya vijijini, pembezoni na yenye changamoto za kijiografia. Kupatikana kwa huduma hizi kunatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi, kijamii na kukuza ujumuishwaji wa kidijitali kwa Watanzania.
Serikali kupitia UCSAF imejipanga kuendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huu hadi kukamilika kwa minara yote, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa.