UJENZI WA MINARA 758 WAFIKIA ASILIMIA 88.39

Mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu unaoendelea kutekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefikia hatua ya kuridhisha, ambapo hadi sasa jumla ya minara 670 kati ya 758 iliyopangwa kujengwa tayari imekamilika. Hii ni sawa na asilimia 88.39 ya utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika kwa wananchi wote, hususan waliopo katika maeneo ya vijijini, pembezoni, na yenye changamoto ya kijiografia. Kupatikana kwa huduma hizi kunalenga kuongeza fursa za kiuchumi, kijamii na kukuza ujumuishwaji wa kidijitali kwa wananchi.
Serikali kupitia UCSAF itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huu hadi kukamilika kwa minara yote, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na huduma bora za mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa.