NAIBU WAZIRI MAHUNDI AWASILIANA NA WANANCHI ZANZIBAR, AHIMIZA MABORESHO YA MAWASILIANO
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameanza ziara ya siku tatu visiwani Zanzibar, ikilenga kuhimiza maboresho ya huduma za mawasiliano katika maeneo yenye changamoto kubwa. Ziara hiyo ilianza tarehe 20 na kukamilika Novemba 23, 2024, ambapo amezuru vijiji mbalimbali katika mikoa ya Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, na Mjini Magharibi.
Katika ziara hiyo, Sheha wa Shehia ya Mchangamdogo, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Asa Makame Said, alieleza furaha ya wananchi wa jimbo la Kojani kufuatia ziara hiyo. Alisema: “Ujio wa Naibu Waziri jimbo la Kojani unatufanya tuwe Watanzania hasa. Asante Rais Samia kuijenga Tanzania moja, hasa kwenye mawasiliano.”
Mkazi wa Shehia ya Kojani, Bi. Timi Ahmed Ali, alieleza kuwa licha ya mawasiliano ya simu za kawaida kuwa mazuri, mtandao wa intaneti bado ni changamoto kubwa na akaomba msaada wa serikali kuboresha huduma hiyo.
Aidha, wananchi wa kisiwa cha Tumbatu katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, walitoa ombi la kuongezewa nguvu kwa minara ya mawasiliano ambayo walisema mara nyingine hushindwa kufanya kazi ipasavyo. Katika kijiji cha Kidunda, ambapo hakuna mawasiliano kabisa, wananchi walionyesha matumaini kuwa changamoto yao itatatuliwa kufuatia ziara hiyo.
Akizungumza na wananchi wa Zanzibar, Naibu Waziri Mahundi alitoa ahadi ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata mtandao bora wa mawasiliano. Alisema: “Upatikanaji wa mtandao utamfikia kila mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kila mmoja aweze kufurahia teknolojia ya mawasiliano.”
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, alieleza kuwa mwaka 2022, serikali ilitoa shilingi bilioni 6.9 kwa ajili ya kuboresha mawasiliano Zanzibar. Fedha hizo zilitumika kujenga minara 42, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto za mawasiliano kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Zanzibar, Bi. Esuvatie Masinga, alisema elimu kwa umma imechangia kupunguza uhalifu wa mitandaoni. Aliweka wazi kuwa kutoka Julai hadi Septemba 2024, mkoa wa Kaskazini Pemba ulikuwa na matukio 15 tu ya ulaghai, huku Kaskazini Unguja yakifika 12. Alihimiza wananchi kuripoti matukio ya utapeli kupitia namba 15040 kwa kuandika neno “TAPELI” likifuatiwa na namba ya mtapeli.
Ziara hiyo ilihusisha mikutano na watoa huduma za mawasiliano, akiwemo Zantel na Tigo, ambapo Naibu Waziri aliwataka kuboresha huduma zao ili kuwafikia Watanzania wote. Alitembelea maeneo sita, yakiwemo Kojani Kisiwani, Kinyikani, Kidundo, na Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba; Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja; Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja; na Kisakasaka Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wananchi wamesema ziara hiyo imeleta matumaini mapya kwa kuboresha mawasiliano visiwani Zanzibar, hatua inayochangia juhudi za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha maendeleo na ushirikiano wa kidigitali nchini.