Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

NAIBU WAZIRI MAHUNDI AKAGUA MINARA YA MAWASILIANO PEMBA, ATAMKA MIKAKATI YA KUBORESHA HUDUMA

Imewekwa: 22 November, 2024
NAIBU WAZIRI MAHUNDI AKAGUA MINARA YA MAWASILIANO PEMBA, ATAMKA MIKAKATI YA KUBORESHA HUDUMA

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Marryprisca Mahundi, amefanya ziara ya kikazi visiwani Pemba kuanzia Novemba 20, 2024, ili kukagua minara ya mawasiliano na kujionea changamoto zilizopo katika sekta ya mawasiliano kwenye maeneo hayo. Ziara hiyo inalenga kuwezesha Serikali kutengeneza mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za mawasiliano kwa wananchi wa Pemba.

Akiwa ameambatana na wataalamu wa sekta ya mawasiliano wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, Mhe. Mahundi pia aliongozana na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ofisi ya Zanzibar, Bi. Esuvatie-Aisa Masinga, pamoja na uwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano Zanzibar.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alitembelea vijiji vya Kojani, Kinyikani, Kidundo, na Wete mjini vilivyopo mkoa wa Kaskazini Pemba. Akiwa katika maeneo hayo, alizungumza na viongozi wa maeneo husika pamoja na wananchi, ambapo walielezea changamoto zao za mawasiliano, zikiwemo ukosefu wa mtandao wa intaneti wenye kasi na mawasiliano ya simu yenye uhakika.

Mhe. Mahundi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinamfikia kila Mtanzania, ikiwemo maeneo ya visiwani kama Pemba. “Huduma za mawasiliano ni nyenzo muhimu ya maendeleo, tunalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata mawasiliano bora na ya uhakika, bila kujali eneo alipo,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Mwasalyanda, alielezea juhudi zinazofanywa na mfuko huo katika kusogeza huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini na visiwani, huku akiahidi kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano katika kushughulikia changamoto zilizoainishwa.

Mhe. Mahundi ameahidi kufuatilia changamoto zote zilizobainishwa na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa haraka, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mawasiliano yanakuwa daraja la maendeleo kwa wananchi wote.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako