SERIKALI YATENGA BILIONI 53 KUIMARISHA MAWASILIANO VIJIJINI NA UBUNIFU WA TEHAMA.
Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kusogeza huduma za mawasiliano karibu na wananchi pamoja na kukuza ubunifu wa teknolojia, baada ya kutenga zaidi ya shilingi bilioni 53 kwa ajili ya miradi ya mawasiliano vijijini na ujenzi wa vituo vya ubunifu vya TEHAMA katika Mwaka wa Fedha 2026/27.
Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki(Mb), wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Kairuki amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 40 zitatumika kuimarisha mawasiliano vijijini kupitia ujenzi wa minara 636 ya simu nchini. Huku akiongeza kuwa mradi huo utalenga kupunguza changamoto za mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara, hususan vijijini, ili wananchi waweze kunufaika na huduma za simu na intaneti kwa urahisi zaidi.
“Tutafanya upembuzi yakinifu katika mikoa yote 31 ili kubaini maeneo yenye changamoto za mawasiliano na kuchukua hatua stahiki,” amesema Kairuki
Mbali na ujenzi wa minara, wizara pia itasimamia utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano ya Simu wa mwaka 2026–2031 pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wanaosimamia miradi hiyo ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
Katika hatua nyingine, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 13.7 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikuu na vituo vidogo vya kuendeleza ubunifu wa TEHAMA (ICT Parks), hatua inayolenga kukuza uchumi wa kidijitali na ajira kwa vijana.
Kupitia vituo hivyo, wananchi watanufaika na mafunzo ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili unde (Artificial Intelligence), pamoja na kuongezewa ujuzi wa kidijitali utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.
Aidha, wizara itaanzisha mpango wa kitaifa wa mageuzi ya kidijitali, kuratibu uanzishwaji wa vituo saba vya ubunifu, na kusimamia programu maalum za kuwawezesha wabunifu na kampuni changa za TEHAMA.
Katika kuimarisha mifumo ya kidijitali, Serikali itafanya kazi ya kuunganisha mifumo 110 ya TEHAMA katika majukwaa ya kitaifa ya kubadilishana data (Data Exchange), hatua itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Hatua hizi zinatarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano na teknolojia nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma, kukuza ubunifu, na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika matumizi ya TEHAMA barani Afrika.