SERIKALI KUPITIA UCSAF YAFIKISHA MAWASILIANO KATIKA VIJIJI 4,041 NCHINI.

  • 09 August, 2024
SERIKALI KUPITIA UCSAF YAFIKISHA MAWASILIANO KATIKA VIJIJI 4,041 NCHINI.

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imefikisha huduma ya mawasiliano ya simu katika vijiji 4,041 vilivyo katika Kata 1,399 kwa kujenga minara 1,532.

Taarifa hiyo imetolewa kwa wananchi waliotembelea banda la UCSAF katika maonesho ya kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama NaneNane yaliyofanyika kitaifa kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2024 katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

UCSAF imeshiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuufahamisha umma kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini  na yasiyo na mvuto wa kibiashara wanafikiwa na huduma za mawasilino.

Tangu kuanzishwa mwaka 2009, Serikali kupitia UCSAF imeingia makubaliano ya kufikisha mawasiliano katika Kata 1,974 zenye vijiji 5,111 kwa kujenga minara 2,185 ya mawasiliano ya simu.

Hivi sasa Serikali kupitia UCSAF inatekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu vijijini, inayojengwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ambapo jumla ya Kata 713 zenye jumla ya vijiji 1,407 zinafikiwa kupitia mradi huu.

Kupitia maonesho hayo, wakulima walipata nafasi ya kufuatilia utekelezaji wa ujenzi wa minara, kuwasilisha changamoto za mawasiliano katika maeneo yao pamoja na kufahamu kwa kina kuhusu majukumu ya UCSAF kwa ujumla.

Serikali inawekeza katika kuboresha mawasiliano kwa kuwa ni nyenzo inayowezesha wakulima kupokea taarifa muhimu kuhusu masuala mbalimbali kama vile; taarifa za hali ya hewa na mbinu bora za kilimo. Kwa kutumia simu za mkononi na redio wakulima wanaweza kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo ni muhimu katika kupanga shughuli zao za kilimo.