Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

SERIKALI KUPITIA UCSAF KUFIKISHA MAWASILIANO KATIKA MAENEO YA KIMKAKATI.

Imewekwa: 24 October, 2025
SERIKALI KUPITIA UCSAF KUFIKISHA MAWASILIANO KATIKA MAENEO YA KIMKAKATI.

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kuanza utekelezaji wa awamu mpya ya ujenzi wa minara 280 ya mawasiliano, ambapo baadhi ya minara hiyo itajengwa katika maeneo ya mipakani, mbuga za wanyama, na njia kuu za reli za SGR na TAZARA.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amebainisha hayo akiwa mkoani Songwe, katika mpaka wa Tanzania na Zambia, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Abdulla, iliyolenga kukagua hali ya mawasiliano katika vijiji vya mipakani vinavyopakana na nchi ya Malawi (wilayani Kyela, mkoani Mbeya) na vile vinavyopakana na Zambia (mkoani Songwe).

Amesema, mradi huo unalenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana katika maeneo yote yenye umuhimu wa kimkakati kwa usalama, utalii, na maendeleo ya taifa.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa minara 758, ambao umefikia zaidi ya asilimia 98 ya utekelezaji, Mhandisi Mwasalyanda, amesema mradi huo unafikia vijiji 1,407 vilivyokuwa havina huduma za mawasiliano kabisa hapo awali, sasa vinafikishiwa huduma hiyo muhimu, hatua inayoboresha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo, ambao sasa wanapata fursa za mawasiliano, huduma za kifedha, elimu kwa njia ya mtandao, biashara mtandao (e-commerce) na huduma nyingine za kidijitali zinazochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, Mhandisi Mwasalyanda amesisitiza kuwa miradi hiyo inaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kujenga Tanzania ya Kidijitali, inayohakikisha wananchi wote wanashirikishwa na kunufaika na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano bila kubakizwa nyuma.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako