Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

KAMATI YA PAC YAPONGEZA UCSAF KUKAMILISHA UJENZI WA MNARA KATA YA MBELEKESE, MKOANI SINGIDA.

Imewekwa: 17 March, 2025
KAMATI YA PAC YAPONGEZA UCSAF KUKAMILISHA UJENZI WA MNARA KATA YA MBELEKESE, MKOANI SINGIDA.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika kusimiamia na kutekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa katika kata 713 zenye vijiji 1,407 nchini kwa lengo la kuboresha huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.  Joseph Kakunda (Mb), baada ya kamati kutembelea na kukagua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa katika kijiji cha Mbelekese, kata ya Mbelekese wilaya ya Iramba Mkoani Singida.

Mnara huu tayari umekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi umejengwa na Kampuni ya simu ya Honora kwa ruzuku ya shilingi milioni 125.2 iliyotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), ni miongoni mwa minara 758 ambayo inaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Tumefika hapa ili kuhakikisha kama kweli mnara huu umewaka na umeanza kutoa huduma, na ndio maana tumetaka pia kusikia kutoka kwa wananchi wenyewe ambao ndio wanufaika. Tumewasikia na tumeridhika na huduma inayopatikana. Tunaipongeza sana Serikali kwa kukakikisha kuwa wananchi wa vijijini wanafikiwa na mawasiliano” amesema.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema, kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758 jumla ya minara 148 inajengwa katika mikoa ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida, Iringa, Tabora na Kigoma. Kati ya hiyo minara 78 imewaka sawa na asilimia 53 ya utekelezaji kwa Kanda ya Kati pekee.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkaguzi Kemi John amesema Ofisi hiyo imejiridhisha kuwa minara 14 kati ya 32 inayojengwa Mkoani Singida imekamilika kwa bajeti iliyokuwa imepangwa na kuwa bado wanafuatilia utekelezaji wa minara mingine 18 inayoendelea kujengwa.

Serikali kupitia UCSAF kwa kushirikiana na makampuni ya simu inatekeleza ujenzi wa minara 758 kwa ruzuku ya shilingi bilioni 126 ili kufikisha mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5 katika kata 713 nchini. Hadi tarehe 14 Machi, 2025 jumla ya minara 425 imewaka na tayari imeanza kutoa huduma, hii ni sawa na asilimia 56.07 ya utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 12 Mei, 2025. Kukamilika kwa mradi huu kutachochea utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidigitali.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako