WAZIRI KAIRUKI ASISITIZA UBUNIFU WA KITEKNOLOJIA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UCSAF
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ubunifu wa kiteknolojia katika utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), akibainisha kuwa ubunifu ni nguzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Mhe. Waziri ametoa kauli hiyo wakati wa ziara maalum ya kikazi katika Ofisi za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na mfuko huo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kairuki ameipongeza UCSAF kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma hizo ili kunufaika na ruzuku za mawasiliano kutoka Serikalini, hasa katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za mawasiliano za uhakika.
Aidha, amehimiza UCSAF kuangalia uwezekano kutumia teknolojia mpya katika utekelezaji wa miradi ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma bora za mawasiliano.
Serikali kupitia UCSAF inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na pembezoni, hatua itakayochangia kuboresha maisha ya wananchi, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha maendeleo jumuishi na endelevu ya sekta ya mawasiliano nchini.
#UCSAF #MawasilianoKwaWote #DigitalEconomy #DigitalTanzania #DigitallyInclusiveTanzania.