Mnara wa mawasiliano ya simu wazinduliwa Longido

  • 06 March, 2023
Mnara wa mawasiliano ya simu wazinduliwa Longido

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb), amefanya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na kampuni ya simu ya MIC Tanzania ( Tigo), kwa ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF).

Katika uzinduzi wa mnara huo uliojengwa katika kijiji cha Noondoto, wilayani Longido Mkoani Arusha, Mhe. Nnauye ameipongeza UCSAF kwa usimamizi mzuri wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini, huku akisisitiza kuwa Serikali  inaendelea kuhakikisha kuwa kila mtanzania bila kujali eneo analoishi anafikishiwa huduma ya mawasiliano.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakere amesema, huduma ya mawasiliano vijijini ni chachu ya maendeleo, hivyo amewataka wanakijiji kuutunza mnara huo kwa manufaa yao.

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema,  UCSAF inatekeleza miradi thelathini na sita (36) katika mkoa wa Arusha ambapo miradi ishirini na saba ( 27), imekamilika na mingine tisa(9) iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Katika mradi huu UCSAF imetoa ruzuku ya zaidi ya shilingi milioni mia moja( 100) ili kufanikisha ujenzi wa mnara huo, ambao utahudumia kijiji cha Noondoto na maeneo ya jirani.