Serikali yaahidi kuendelea kuiimarisha UCSAF

  • 10 January, 2023
Serikali yaahidi kuendelea kuiimarisha UCSAF

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), Serikali itaendelea kuimarisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) ili uweze kuhakikisha kuwa huduma bora za mawasiliano zinawafikia wananchi wote hasa waishio pembezoni mwa nchi.

Mhe Nnauye ameyasema hayo wakati akizindua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kata ya Inyonga Wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Mnara huo umejengwa kupitia ruzuku inayotolewa na UCSAF.

Amesema, Serikali inatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na UCSAF kwani bila Mfuko huo huduma ya mawasiliano isingeweza kufika maeneo ya vijijini. Aidha ametoa rai kwa wananchi kutambua juhudi hizo na kuhakikisha kuwa wanalinda miundombinu ya mawasiliano ambayo inawekezwa katika katika maeneo yao.

Katika uzinduzi huo Mbunge wa Jimbo la Mlele Bw. Isaac Kamwelwe ameishukuru Serikali kupitia UCSAF kwa kushirikiana na TTCL katika ujenzi wa mnara huo

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi, Peter Ulanga amesema mnara huo umejengwa ili kuiongezea nguvu minara mingine mitano (5) iliyopo katika wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba amesema kwa Mkoa wa Katavi pekee, ruzuku iliyotolewa na Serikali kupitia Mfuko huo ni shilingi bilioni sita ambayo imetumika kujenga minara 37, thelathini kati ya hiyo imekamilika na mingine saba inaendelea kujengwa.