Serikali yadhamiria kumaliza tatizo la usikivu wa radio ifikapo 2025
- 15 September, 2021
Kutokana na kuwepo kwa changamoto ya usikivu wa Redio ya Taifa kwa baadhi ya maeneo nchini hususani maeneo ya Mipakani mwa nchi, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi ya kuboresha usikivu wa raidio katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa kushirikiana na shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imejikita katika kuhakikisha huduma ya utangazaji inawafikia wananchi wengi zaidi kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya kurushia matangazo katika studio za redio ya Taifa katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwemo ya mipakani.
Akizindua kituo cha kurushia matangazo ya TBC Taifa na TBC FM kilichojengwa na UCSAF katika kijiji cha Sesenga, wilayani Morogoro, Mkoani Morogoro, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Dkt. Faustine Ndugulile amesema Serikali Kupitia Mfuko huo imejielekeza katika kumaliza kabisa tatizo la usikivu wa radio na simu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo ya pembezoni na mipakani mwa nchi ifikapo mwaka 2025.
Ujenzi wa kituo hicho umetanguliwa na ujenzi, ukarabati uaiznduzi wa Studio za radio Jamii Mkoani Dodoma na Arusha. Kituo hicho cha kurushia matangazo utakuwa na manufaa kwa eneo la kimkakati la bwala la Mwalimu Nyerere, wanananchi wa maeneo hayo pamoja na maeneo mengine ikiwemo mbuga ya Selous, kwa kuwa wataanza kupokea matangazo ya TBC Taifa na TBC FM.
Ili kuboresha mawasiliano ya simu na huduma zingine za utangazaji katika eneo hilo, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unakusudia kufanya mazungumzo na makampuni ya simu pamoja na watoa huduma za utangazaji kutumia mnara mpya uliopo katika eneo la Sesenga ili kutoa huduma hizo muhimu kwa wananchi.
Hadi sasa asilimia 66 ya maeneo ya kijeografia nchini yanapata huduma ya mawasiliano lengo likiwa ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2025. Kwa upande mwingine matumizi ya intaneti kwa sasa ni asilimia 43 lengo ni kufikia asilimia 100 pia ifikapo 2025.
Makubaliano kati ya UCSAF na TBC hayahusisha ujenzi wa vituo vipya,ukarabati za studio za zamani na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa. Maeneo mengine yatakayonufaika pamoja na Ruangwa - Lindi, Kyela – Mbeya, Ngara na Kyerwa – Kagera, Ludewa – Njombe, Tanganyika - Katavi, Uvinza - Kigoma, Makete - Njombe na Mbinga- Ruvuma.