KAMATI YA UKAGUZI YA WIZARA YA HABARI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA MRADI WA MINARA YA MAWASILIANO VIJIJINI
Kamati ya Ukaguzi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya ziara ya kukagua miradi ya minara ya mawasiliano vijijini na kujionea maendeleo mazuri ya miradi hiyo ambayo wananchi wameshaanza kunufaika kwa kupata huduma za mawasiliano ya uhakika.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Bw. Mulembwa Munaku, amesema Serikali kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliingia mkataba kwa kipindi cha miaka miwili cha ujenzi wa minara 758, ambapo tukio la uzinduzi lilishuhudiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 na utekelezaji wake ulianza mwaka 2023 hadi 2025.
Kamati hiyo imefanya ziara kwa siku mbili Novemba 11 na 12, 2024 katika wilaya za Dodoma, ikiwa ni pamoja na Chemba, Bahi, Chamwino, Kondoa, Kongwa na Dodoma Mjini, na kukagua jumla ya miradi ya minara 17 ambayo imekamilika na imeanza kutoa huduma japokuwa kuna baadhi inaendelea kumalizia ujenzi wa uzio na nyumba za walinzi.
“Minara hii yote inatoa huduma za mawasiliano kwa teknolojia ya kisasa ya 3G na 4G, hali inayowawezesha wananchi katika maeneo hayo kupata huduma za intaneti pamoja na faida nyingine za matumizi ya mtandao”, amezungumza Bw. Munaku
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo, walielezea kutambua kuwa bado kuna maeneo magumu kufikika kutokana na kukosekana kwa barabara na kushauri Mamlaka husika, wananchi, na makampuni ya simu kushirikiana kwa ukaribu ili kumaliza changamoto hizo na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imepongeza jitihada za Serikali za kutoa ruzuku kwa makampuni ya simu ili yachukue hatua za kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya vijijini, ambayo kibiashara hayakuwa rahisi kufikiwa.
Wananchi walionufaika na huduma za mawasiliano walieleza furaha yao na kuipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa kuwafikishia huduma hiyo muhimu ambayo inarahisisha uendeshaji wa shughuli zao za kila siku.