Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA TEHAMA 2026/27.

Imewekwa: 30 April, 2026
MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA TEHAMA 2026/27.

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) imepanga kutekeleza miradi mikubwa ya kuboresha mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini katika Mwaka wa Fedha 2026/27, hatua inayolenga kupunguza pengo la kidijitali kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki(Mb), wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kairuki amesema kuwa UCSAF itaelekeza nguvu katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote bila kujali mahali walipo.

Katika mpango huo, ujenzi wa minara ya mawasiliano utakamilishwa katika kata 567 ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za simu na intaneti. Hatua hii inatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo hayo.

Pia, Mhe. Kairuki ameongeza kuwa, Serikali imepanga kuboresha usikivu wa Redio ya Taifa (TBC) katika mikoa ya Manyara, Mtwara, Mwanza, Ruvuma na Kilimanjaro, ili kuhakikisha wananchi wanapata habari na taarifa muhimu kwa wakati.

Kwa upande wa sekta ya posta, vituo 31 vya huduma vitaanzishwa huku vifaa vya kisasa vya TEHAMA vikisambazwa ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hizo. Aidha, huduma ya intaneti ya wazi (Wi-Fi) itaunganishwa katika maeneo 100 ya umma nchini ili kurahisisha upatikanaji wa mtandao kwa wananchi.

Katika kukuza elimu ya TEHAMA, maabara za kompyuta zitajengwa katika shule 250 za umma, huku shule 10 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu zikipewa vifaa maalum vya TEHAMA ili kuwajengea mazingira bora ya kujifunza.

Vilevile, miundombinu ya TEHAMA itajengwa katika vyuo 15 vya mafunzo ya ufundi, sambamba na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 700 na wanafunzi 250 wa kike, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia.

Amesema  utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kuimarisha elimu ya kidijitali, na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kwa ujumla.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako