Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

UCSAF YALENGA WANANCHI KUFIKIWA NA MAWASILIANO IFIKAPO 2030.

Imewekwa: 06 October, 2026
UCSAF YALENGA WANANCHI KUFIKIWA NA MAWASILIANO IFIKAPO 2030.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhe. Balozi Valentino Mlowola, amesema UCSAF inalenga kuhakikisha wananchi wote Tanzania wanafikiwa na huduma za mawasiliano ifikapo mwaka 2030, sambamba na juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Mhe. Mlowola ameyasema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za sekondari nchini, akieleza kuwa jukumu kubwa la Bodi ni kuhakikisha UCSAF inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, maelekezo ya Serikali na matarajio ya wananchi wanaonufaika na huduma zinazowezeshwa na Mfuko.

Amesema UCSAF imepata mafanikio makubwa ambapo imeingia katika orodha ya taasisi 10 bora katika makundi matatu kati ya manne, miongoni mwa taasisi 250 zilizo chini ya Serikali Kuu. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa sera za Serikali, usimamizi wa Bodi pamoja na utendaji wa Menejimenti na watumishi wa UCSAF.

Aidha, amesema UCSAF haijajikita katika kuwezesha upatikanaji wa miundombinu ya mawasiliano pekee, bali pia inawezesha upatikanaji wa vifaa na mafunzo ya TEHAMA kwa walimu na wanafunzi, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kutumia teknolojia na kunufaika na fursa za uchumi wa kidijitali.

Mhe. Mlowola ametoa shukrani kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, viongozi wa Bodi, vyuo vinavyoshiriki katika programu hiyo, Menejimenti ya UCSAF, walimu na watumishi kwa ushirikiano wao, huku akisisitiza kuwa UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha lengo la wananchi wote kufikiwa na huduma za mawasiliano ifikapo mwaka 2030.

#UCSAF #MawasilianoKwaWote #MafunzoYaTEHAMAkwaWalimu2026

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako