Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

UCSAF NA TBC WASAINI HATI YA MAKUBALIANO KUIMARISHA REDIO JAMII

Imewekwa: 07 September, 2026
UCSAF NA TBC WASAINI HATI YA MAKUBALIANO KUIMARISHA REDIO JAMII

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) wamesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuimarisha uanzishaji, uendelezaji na uendelevu wa vituo vya redio jamii vinavyofadhiliwa kupitia ruzuku ya UCSAF.

Hati hiyo imesainiwa leo jijini Dar es Salaam kati ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bw. Mulembwa Munaku, na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Bi. Asha Dachi, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa taasisi hizo katika kuhakikisha wananchi, hususan waliopo maeneo ya vijijini na yenye changamoto za miundombinu ya utangazaji, wanapata huduma za mawasiliano na taarifa.

Kupitia makubaliano hayo, TBC itatoa utaalamu wa kiufundi katika uanzishaji, ujenzi na uendelezaji wa vituo vya redio jamii pamoja na minara ya kurushia matangazo, ikiwemo kutoa mafunzo kwa waendeshaji wa vituo hivyo. Lengo ni kuhakikisha miundombinu inayowekezwa kupitia fedha za Serikali inatumika kwa ufanisi na vituo vinaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.

Hadi sasa UCSAF imewezesha kuanzishwa kwa vituo vitano vya redio jamii kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 3, huku ushirikiano wake na TBC wa takribani miaka 10 ukiwa umehusisha jumla ya shilingi bilioni 16.93 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kuongeza usikivu wa redio ya Taifa na kuboresha huduma za utangazaji. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 15.3 zimetengwa kwa utekelezaji wa miradi 37 ya kuongeza usikivu wa redio ya Taifa, huku shilingi bilioni 3.3 zikitengwa katika mwaka wa fedha 2026/27.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya UCSAF na TBC katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa mawasiliano na taarifa, sambamba na kuchangia juhudi za Serikali za kujenga Tanzania yenye mawasiliano jumuishi.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako