UCSAF YAJIVUNIA MIAKA MINNE YA DKT SAMIA KATIKA KUBORESHA SEKTA YA MAWASILIANO NCHINI.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya mawasiliano nchini, kupitia ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha miundombinu ya mawasiliano, hasa katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa UCSAF katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mhandisi Mwasalyanda amesema kuwa UCSAF imekamilisha ujenzi wa jumla ya minara 1,783 katika vijiji 4,482, hatua ambayo imewezesha zaidi ya wananchi milioni 24 kupata huduma za mawasiliano.
Aidha kwa upande wa Zanzibar, Serikali kupitia UCSAF imekamilisha ujenzi wa minara 42 ya mawasiliano katika shehia 38 za Unguja na Pemba kwa gharama ya shilingi bilioni 6.9. Mradi huu unalenga kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar, hasa wale walioko katika maeneo ya mbali, kuhakisha kuwa wanapata huduma bora za mawasiliano, jambo ambalo awali lilikuwa ni changamoto. Minara hii inarahisisha mawasiliano kwa wananchi na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile elimu, afya, na biashara, ambazo hutegemea mawasiliano ya haraka.
Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano. Serikali inaendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kuwezesha wananchi wote kufikiwa na huduma za mawasiliano.
Huu ni mchakato wa kipekee utakaosaidia wananchi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kuongeza ufanisi wa shughuli za Utekelezaji wa miradi hii ya UCSAF unaonesha mafanikio makubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wote, huku Serikali ikiendelea kutoa kipaumbele kwa kuboresha miundombinu ya mawasiliano kama moja ya vipaumbele vya msingi vya Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidigitali, hii ikiwa ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo endelevu katika nchi, kwa kusaidia kukuza biashara, elimu, na huduma za afya.