UCSAF YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KWA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekabidhi vifaa vya TEHAMA vikiwemo Personal Digital Assistants (PDA), kompyuta na vifaa vingine kwa Shirika la Posta Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za mawasiliano na posta nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa, alisema hatua hiyo inalenga kuifanya Posta kuwa taasisi ya kisasa inayotoa huduma bora, nafuu na jumuishi kwa wananchi wote.
“Serikali ya Awamu ya Sita imeweka wazi msimamo wake kuwa huduma za posta, mawasiliano na huduma za kifedha za kidijitali si anasa bali ni haki ya kila Mtanzania. Vifaa hivi vitaiwezesha Posta kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, wakiwemo wakulima, wavuvi na wafanyabiashara,” alisema Mhe. Silaa.
Kwa mujibu wa Waziri, vifaa hivyo vitasaidia kuongeza uwazi, kupunguza ucheleweshaji na kuongeza ufanisi wa Shirika la Posta Tanzania. Aidha, vifaa hivyo pia vitaboresha kasi ya usambazaji wa barua na vifurushi, sambamba na kufungua milango ya huduma mpya za biashara mtandaoni, malipo ya kidijitali na huduma za Serikali mtandao.
Mhe. Silaa aliipongeza UCSAF kwa kusema kuwa, huu ni mfano bora wa mshikamano wa kitaasisi huku akisisitiza kuwa Serikali itabaki thabiti katika kuhakikisha sekta ya Posta na mawasiliano inaendelea kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali.