UCSAF YAKUTANA NA VYUO VIKUU KUJADILI USHIRIKIANO KATIKA UTAFITI WA MIRADI YA MAWASILIANO
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umekutana na wawakilishi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kujadili fursa za ushirikiano katika kufanya tafiti zinazohusiana na utekelezaji wa miradi ya mawasiliano, hususan katika maeneo yanayonufaika na miradi ya UCSAF.
Taasisi zilizoshiriki katika mazungumzo hayo ni Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) pamoja na Chuo cha Teknolojia Arusha.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zimejadili namna ya kuunganisha utaalamu na rasilimali zilizopo ili kufanya tafiti zitakazosaidia kutathmini matokeo ya miradi ya UCSAF, kubaini mahitaji ya wananchi na kupima mchango wa huduma za mawasiliano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, ushirikiano huo unalenga kutoa fursa kwa wahadhiri na wanafunzi kushiriki katika tafiti za kitaaluma zinazohusiana na sekta ya mawasiliano na TEHAMA, pamoja na kuchochea ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo ya vijijini na pembezoni.
Kupitia ushirikiano huo, UCSAF inalenga kutumia matokeo ya tafiti za kisayansi kama msingi wa kuboresha upangaji, utekelezaji na tathmini ya miradi yake ili kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano unaleta matokeo yenye manufaa kwa wananchi.