UCSAF Yaandaa Mafunzo ya TEHAMA kwa Wanafunzi wa Kike Kuadhimisha Siku ya Wasichana na TEHAMA 2025

Katika kuadhimisha siku ya wasichana na TEHAMA (International Girls in ICT Day) 2025, Mfuko kwa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeandaa mafunzo maalum kwa wanafunzi wa kike wa shule za Sekondari za Umma nchini, ambapo jumla ya wananfunzi 248 kutoka mikoa yote ya Tanzania na Zanzibar wanatarajiwa kushiriki katika mafunzo haya.
Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka na yanalenga kuhamasisha wasichana kuchagua masomo na taaluma katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati yaani STEM, lengo kuu likiwa ni kuvunja vikwazo vya kijinsia na kubaini uwezo wa wanawake na wasichana katika sekta ambazo zimekuwa zikionekana ni ngumu kwao.
Mafunzo haya yanafanyika katika vituo sita ambavyo viko Zanzibar, Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya ambapo wanafunzi watajengewa ujuzi wa kidigitali kwa kufundishwa masuala ya coding, digital skills, robotics na matumizi ya TEHAMA katika kutatua changamoto za kijamii.
Katika maadhimisho ya 2025, Serikali, taasisi za elimu, mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo wameweka mikakati ya kupunguza vikwazo hivi na kuhakikisha kuwa wasichana wanayapenda masomo ya STEM.