UCSAF YATUNUKIWA TUZO YA GIRLS IN ICT CHAMPION AWARD
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetunukiwa tuzo ya Girls in ICT Champion Award kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza mradi wa Girls in ICT, unaolenga kuwahamasisha wanafunzi wasichana kupenda na kuchagua masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Tuzo hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Poland, Daria Jankiel, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 10 ya Kampuni ya Transfer Multisort Elektronik (TME) ya nchini Poland.
Kupitia mradi wa Girls in ICT, UCSAF imekuwa ikitoa mafunzo na kuwawezesha wasichana kupata uelewa na ujuzi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuwahamasisha kujenga shauku na kujiunga na taaluma zinazohusiana na STEM.
Tuzo hiyo imepokelewa na Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Richard Sotery, akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa UCSAF.