UCSAF YAJIZATITI KUIMARISHA MAWASILIANO MIPAKANI KWA KUSHIRIKIANA NA TBC

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itaendelea kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kuhakikisha wanaboresha na kujenga vituo vya redio katika maeneo mbalimbali nchini hasa ya mipakani.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi na kuboresha usikivu wa matangazo ya redio za TBC ili kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo ambayo hawapati huduma hiyo.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara fupi katika studio za TBC Redio Jamii na Studio za TBC1 Kanda ya Makao Makuu Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF Balozi Valentino Mlowola amesema ni fursa kwa wananchi kwenda kisasa na kukua kupitia mawasiliano kwa njia ya redio.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema dhamira ya shirika hilo ni kutatua changamoto ya usikivu katika maeneo ya mipakani.
Usikivu wa redio za TBC kote nchini kwa sasa umeongezeka na kufikia asilimia 92 kutoka asilimia 54 mwaka 2016, hatua hiyo imefikiwa kutokana na ushirikiano kati ya UCSAF na TBC.