Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

UCSAF YAPANGA AWAMU MPYA YA UJENZI WA MINARA 280 KUFIKISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO VIJIJINI

Imewekwa: 01 October, 2025
UCSAF YAPANGA AWAMU MPYA YA UJENZI WA MINARA 280 KUFIKISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO VIJIJINI

Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), umetangaza kuanza ujenzi wa minara mingine 280 katika awamu ya 10 ili kuifungua Tanzania katika mawasiliano hasa maeneo ambayo yalikosa huduma hiyo.

Kabla ya kuanza kwa ujenzi wa minara hiyo, UCSAF kwa sasa inandelea na ujenzi wa minara 758 ambayo utekelezaji wake upo kwa asilimia 97 hivyo ujenzi wa minara mipya utafikisha jumla ya minara 1,038 iliyojengwa katika kipindi kifupi.

Katika taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa UCSAF Peter Mwasalyanda alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Pemba wilayani Mvomero, Morogoro, amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa minara 758, wataanza kujenga kwa haraka minara mingine 280 ambayo hatua zote zimeshakamilika.

Amesema UCSAF inajenga minara katika maeneo yenye changamoto za kijiografia, jambo alilodai limekuwa kikwazo katika kufikia kasi ya ujenzi inayotakiwa hasa wakati wa upelekeaji wa malighafi.

“Hata hivyo, UCSAF imeweka mikakati thabiti kuhakikisha kila awamu inakamilika kwa wakati, ili huduma zipatikane kwa idadi kubwa ya wananchi, na tumekuwa tukifuatilia hatua kwa hatua kwa wasimamizi wa ujenzi huo kwani wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa mawasiliano hayo,” amesema Mwasalyanda.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu, ujenzi mwingine wa minara awamu ya 11 utaanza mara baada ya kukamilisha ujenzi wa minara 280 ambapo awamu hiyo pia itakwenda kujengwa minara 280 na kwamba miradi yote hiyo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.

Walengwa zaidi ni wananchi walioko vijijini na pembezoni, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa lakini kuwa na mawasiliano na ndugu na jamaa zao kwani upatikanaji wa huduma za mawasiliano ni haki ya kila mwananchi bila kujali anaishi kwenye mazingira yapi.

UCSAF pia imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano, wananchi na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha utekelezaji wenye tija na endelevu ikiwemo kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku na kuchangia ukuaji wa Taifa.

Diwani aliyemaliza muda wake kata ya Pemba Coster Reuben amekiri hali ilikuwa ngumu kwenye masuala ya mawasiliano kabla ya kuanza kwa ujenzi wa minara na mara nyingi hata usalama wa wananchi ulikuwa mdogo kwani hawakuwa wakitoa taarifa kwa wakati pindi yanapotokea matukio jambo lililopelekea vyombo vya ulinzi kutofika kwa wakati.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako