Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

UCSAF KUJENGA MAABARA 250 ZA TEHAMA SHULENI.

Imewekwa: 06 October, 2026
UCSAF KUJENGA MAABARA 250 ZA TEHAMA SHULENI.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unatarajia kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa maabara 250 za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shule mbalimbali za umma nchini katika mwaka huu wa fedha, ikiwa ni hatua mpya ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika elimu.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bw. Mulembwa Munaku, ameyasema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za sekondari nchini, yaliyofunguliwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki ( Mb.)

Amesema utekelezaji wa mpango huo utahusisha kufikisha maabara kamili za TEHAMA zenye kompyuta 20 kwa kila shule itakayofikiwa na mradi huo, hatua inayolenga kuongeza fursa kwa wanafunzi na walimu kutumia teknolojia kwa vitendo katika ufundishaji na ujifunzaji.

Ameeleza kuwa utaratibu huo ni tofauti na ule wa awali ambapo UCSAF ilikuwa ikifikisha kompyuta chache, takribani tano kwa shule. Kupitia utaratibu mpya, shule zitakazofikiwa zitawekewa maabara kamili, ikiwemo kufungwa vifaa na kuwekwa katika mazingira yatakayowezesha matumizi yake kwa ufanisi.

Hatua hiyo inaendeleza uwekezaji wa UCSAF katika TEHAMA ambapo hadi sasa zaidi ya shule 1,121 zimewezeshwa vifaa mbalimbali, ikiwemo kompyuta, projektor na printa. Aidha, mafunzo yanayotolewa kwa walimu yanalenga kuwajengea uwezo wa kutumia TEHAMA katika ufundishaji pamoja na kutunza vifaa hivyo ili viweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Kwa upande wa miundombinu ya mawasiliano, Bw. Munaku amesema UCSAF kupitia ruzuku inayotolewa kwa Kampuni za Mawasiliaino ya simu imewezesha ujenzi wa minara 2,166 katika kata 2,306 nchini, ambayo imekamilika na inaendelea kutoa huduma kwa wananchi. Amesema hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Mfuko za kupanua upatikanaji wa mawasiliano na TEHAMA na kuchangia kupunguza pengo la kidijitali nchini.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako