UCSAF yatoa msaada kwa Hospitali ya Mirembe

  • 25 March, 2022
UCSAF yatoa msaada kwa Hospitali ya Mirembe

Ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umesherehekea siku ya wanawake duniani kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula na taulo za kike kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya afya ya akili Mirembe.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo yenye thamani ya sh. Milioni 3.5, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashimba amesema, imekuwa ni utaratibu wa UCSAF kuyakumbuka na kuyafikia makundi maalum yenye uhitaji kwa sababu ni njia mojawapo ya kuonyesha uwajibikaji kwa jamii.

Mashiba ametoa wito kwa watu binafsi na taasisi nyingine za binafsi na za umma kusaidia hospitali hiyo, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa ambao baadhi yao wametelekezwa na familia zao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dkt. Paul Lawala ameishukuru UCSAF kwa kukumbuka wahitaji waliopo katika hospitali hiyo huku akiongeza kuwa msaada huo ni wa muhimu sana na utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za upatikanaji wa chakula kwa wagonjwa.

Vifaa vilivyotolewa hospitalini hapo ni pamoja na mchele kilo 500, maharage kilo 200, unga wa ngano kilo 125, sukari kilo 160, mafuta ya kula lita 120 pamoja na taulo za kike katoni 50.