Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

Bodi ya Tume ya Mawasiliano Uganda yafanya ziara ya mafunzo- UCSAF

Imewekwa: 27 June, 2025
Bodi ya Tume ya Mawasiliano Uganda yafanya ziara ya mafunzo- UCSAF

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umepokea ugeni kutoka Bodi ya Tume ya Mawasiliano ya Uganda (Uganda Communications Commission - UCC) waliokuwa katika ziara rasmi ya mafunzo nchini Tanzania, yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini.

Wajumbe wa bodi hiyo waliongozwa na Mwenyekiti wao, Dkt. Charity Baseball Mulenga. Wakiwa jijini Dodoma, walitembelea makao makuu ya UCSAF na kupokelewa rasmi na Menejimenti ya Mfuko ikiongozwa na Kaimu Mtendaji Mkuu, Mhandisi Albert Richard, pamoja na timu ya wataalamu wa UCSAF.

Katika mazungumzo yao, UCSAF iliwasilisha kwa undani mafanikio ya Mfuko katika kupanua huduma za mawasiliano vijijini, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa minara ya mawasiliano, usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shule za umma, pamoja na miradi ya mawasiliano kwa jamii maalum kama vile walemavu na vituo vya afya.

Aidha, UCSAF ilielezea mikakati yake ya muda mrefu ya kuhakikisha Watanzania wote, bila kujali eneo walilopo, wanapata huduma za mawasiliano kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi. Mikakati hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha ajenda ya Serikali ya Tanzania ya kujenga uchumi wa kidijitali unaojumuisha wananchi wote.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa UCC, Dkt. Mulenga alielezea kufurahishwa kwake na kiwango cha maendeleo ya miradi ya UCSAF, akisisitiza kuwa Tanzania imeweka mfano mzuri wa namna taasisi za umma zinavyoweza kusimamia kwa ufanisi miradi ya kuunganisha wananchi kupitia teknolojia ya mawasiliano. Alibainisha kuwa mambo mengi waliyojifunza katika ziara hiyo yatatumika kama rejea katika kuboresha mifumo ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini Uganda.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi za kukuza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya mawasiliano, ambapo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Mashariki na Kusini mwa Afrika zinahamasishwa kubadilishana uzoefu, kujifunza kwa pamoja, na kuimarisha juhudi za pamoja katika kujenga miundombinu ya TEHAMA kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, UCSAF imeelezea nia yake ya kuendeleza ushirikiano huu, huku ikisisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya mawasiliano katika Afrika yanahitaji mshikamano wa kweli, ubunifu wa pamoja na maamuzi ya kimkakati yanayolenga kuinua maisha ya wananchi wote.

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako