Waziri Kijaji awataka walimu waliopata mafunzo ya TEHAMA kutoa elimu hiyo kwa walimu wenzao.

  • 28 October, 2021
Waziri Kijaji awataka walimu waliopata mafunzo ya TEHAMA kutoa elimu hiyo kwa walimu wenzao.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka walimu waliopata mafunzo ya TEHAMA watakaporudi katika vituo vyao vya kazi, kuwafundisha walimu wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo ili kuleta chachu kwa walimu wengi zaidi katika kuleta mabadiliko ya ufundishaji katika shule zao.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo katika kituo cha Dar es salaam (DIT), yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Taasisi yaTeknolojia ya Dar es salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ambapo jumla ya walimu 650 wamenufaika na mafunzo hayo kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara, na mikoa 5 ya Zanzibar.

Waziri, Dkt. Kijaji ameupongeza uongozi wa UCSAF DIT, UDOM na MUST kwa kusimamia uendeshaji wa mafunzo hayo kwa umahiri, huku akiongeza kuwa  shule nyingi za serikali zimekuwa uhaba wa vifaa vya TEHAMA na hivyo kuwafanya wanafunzi kuwa nyuma katika masuala ya kidigitali.

“Tunatambua kuwa TEHAMA ndio kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na mabadiliko ya kijamii duniani kote. TEHAMA inasaidia katika masuala ya ufundishaji na ujifunzaji kupitia mbinu mbalimbali kama vile kubadilisha matumizi ya chaki na kutumia projekta, pia inawapa uwezo wanafunzi kutazama mihadhara wakiwa kwenye Kompyuta hasa katika vipindi vya majanga kama ilivyotokea mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19” amesema Dkt. Kijaji

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UCSAF Profesa John Nkoma, akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Mfuko, amemshukuru Waziri Dkt. Kijaji kwa kukubali mwaliko wa kufunga mafunzo hayo na kuahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Mfuko.

Nae Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba ametoa wito kwa walimu kuitumia vyema elimu waliyopata ili kupunguza gharama  zisizo za lazima za matengenezo ya vifaa vya TEHAMA, na kuongeza kuwa ujuzi walioupata unatosha kuwawezesha kufanya marekebisho ya vifaa hivyo kila mara vinapokuwa na matatizo madogo madogo ya kiufundi.