WAZIRI NAPE AZINDUA KAMPENI YA ELIMU KWA UMMA KUHUSU MINARA 758

  • 26 January, 2024
WAZIRI NAPE AZINDUA KAMPENI YA ELIMU KWA UMMA KUHUSU MINARA 758

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye (Mb), amezindua kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini unatekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo, Waziri Nape ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za mawasiliano ya simu (sauti na intaneti/data) zinapatikana kote nchini.

Akizindua Kampeni hiyo yenye lengo la kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa mradi huo, amewataka viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma waliohudhuria uzinduzi kuwa mabalozi wazuri wa Serikali kwa kuisemea vema kwa wananchi.

Amesema moja kati ya hatua muhimu iliyofikiwa hadi sasa ni pamoja na kutolewa kwa vibali vyote vya ujenzi wa minara 758, hatua ambayo imewezesha kuanza kwa ujenzi wa minara katika maeneo ya utekelezaji wa mradi.

Aidha ameongeza kuwa, hadi kufikia tarehe 24 Januari, 2024 jumla ya minara tisa (9) ilikuwa imekamilika na tayari imewashwa wakati minara mingine 85 inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari, 2024.

Serikali iliingia pia makubaliano ya kuiongezea nguvu(upgrade) jumla ya minara 304 iliyokuwa inatoa huduma kwa teknolojia ya 2G pekee(sauti). Hadi sasa minara 190 kati ya hiyo ineongezewa nguvu na inatoa huduma kwa teknolojia kwa teknolojia ya 3G na 4G. (sauti na data/ intaneti).