Minara 77 kuongezewa uwezo wa 3G kwa ajili ya intaneti

  • 15 September, 2021
Minara 77 kuongezewa uwezo wa 3G kwa ajili ya intaneti

Katika hatua nyingine serikali  kupitia Mfuko wa Mawasiliano imekamilisha zoezi la kusaini mikataba ya miradi ya kuiongezea uwezo (upgrade) minara 77 katika kata 77 zenye uwezo wa kutoa huduma kwa kiwango cha 2G ili itoe huduma ya intaneti kwa kiwango cha 3G. Mikataba iliyokamilishwa ni baina ya Mfuko na kampuni za Airtel, Vodacom na MIC. Kupitia mradi huu, Vodacom inaongezea uwezo (upgrade) minara 20, Airtel minara 37 na MIC minara 20. Aidha, Mfuko uko katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za manunuzi ili kutia saini mikataba ya kuiongezea uwezo minara 50 iliyojengwa na TTCL.

Mradi huu utaongeza matumizi ya intaneti katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 ambayo katika kipengele namba 60 inaelekeza kuimarisha mfumo wa TEHAMA wa kudhibiti usalama na mapato katika mawasiliano. Kadhalika, kuongeza mchango wa sekta ya mawasiliano kwenye Pato la Taifa kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA, ikiwemo kubuni na kutekeleza mikakati ya kuweka mazingira bora ya ushindani na udhibiti katika sekta ya mawasiliano ili wananchi wengi Zaidi wamudu gharama za mawasiliano. 

Vile vile kuongeza wigo na matumizi ya mawasiliano ya kasi (broadband) kutoka asilimia 45 mwaka 2020 hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 na kuongeza watumiaji wa intaneti kutoka asilimia 43 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2025. Zaidi, Ilani inaelekeza kuanzisha huduma za mawasiliano za intaneti ya kasi (broadband) katika maeneo ya umma (public places) ikiwamo maeneo ya hospitali, taasisi za elimu na vituo vya usafiri hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2025, kuunganisha taasisi za serikali na miundombinu ya mtandao wa kasi kufikia asilimia 70 na kuboresha huduma za mawasiliano ya simu za viganjani ili kupatikana maeneo yote.