Serikali yadhamiria kuboresha mawasiliano ya simu na intaneti nchini

  • 14 December, 2021
Serikali yadhamiria kuboresha mawasiliano ya simu na intaneti nchini

Serikali imedhamiria kufikisha huduma za mawasiliano ya simu na intaneti ya kasi kwa kila mtanzania kwa asilimia 100 ndani ya kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya sitini na Ibara ya sitini na moja ambazo zinaitaka Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa watanzania wote wanafikiwa na huduma hiyo muhimu
ili kutatua kero ya ukosefu wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasilino na Teknolojia ya Habari, Mhe, Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa katika Kijiji cha Matuli, Kata ya Matuli, Wilaya ya Morogoro vijijini Mkoani Morogoro, ambako kwa muda mrefu wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitumia “Mti wa mtandao” ambapo walifunga makopo waliyatumia kuweka simu zao ili ziweze kupata mtandao. 

Mnara huo wenye uwezo wa kutoa huduma kwa teknolojia ya 2G,3G na 4G umejengwa na kampuni ya simu ya Airtel kupitia ruzuku ya milioni 125 iliyotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Dkt. Kijaji amesema kuwa ujenzi wa mnara huo utawezesha upatikanaji wa uhakika wa mawasiliano ya simu na intaneti, pia utachangia katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kupata taarifa zinazohusu kilimo, uuzaji wa mazao na upatikanaji wa masoko kwa kutumia simu ya kiganjani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigella ameishukuru Serikali kupitia UCSAF kwa kuona umuhimu wa kutatua kero ya mawasiliano ya muda mrefu katika eneo hilo. Amesema kupatikana kwa huduma hiyo katika Kata ya matuli kutachangia maendeleo ya wananchi.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Wakili Alberto Msando ametoa maelekezo kwa kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa miundombinu katika mnara huo inakuwa na ulinzi muda wote ili kuepuka uharibifu na wizi kutokea katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mhe, Hamis Talelate ameishukuru UCSAF kwa ujenzi wa mnara huo huku akisisitiza kuwa ataendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali katika eneo Kata hiyo.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema uzinduzi wa mnara huo ni muendelezo wa utekelezaji wa makujumu ya UCSAF katika kuhakikisha kuwa kila mtanzania anafikiwa na huduma bora za mawasiliano bila kujali anaishi mjini ama kijijini.