UCSAF Kuboresha Huduma Za Utangazaji Mikoa Saba

  • 16 February, 2023
UCSAF Kuboresha Huduma Za Utangazaji Mikoa Saba

 

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kutekeleza mradi wake wa kuboresha huduma za utangazaji katika mikoa saba nchini ambapo maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni pamoja na Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Ileje, Mtama, Same, Kilindi, Mbulu na Rufiji.

Mtandaji  Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba  amesema; “UCSAF itajenga mnara mmoja kwa kila Halmashauri kwa ajili ya redio jamii na mkataba kwa maeneo haya Saba tayari umesainiwa ambao unagharimu shilingi bilioni 2.1, ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 utekelezaji wake utaanza katika Wilaya ya Arusha DC, Mpimbwe Mkoani Katavi, Bariadi Mkoa wa Simiyu na Biharamulo mkoani Kagera,” amesema Mtendaji Mkuu Mashiba.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa, kuhusu kuboresha usikivu wa redio ya Taifa TBC, UCSAF inashirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuboresha usikivu wa matangazo yake ambapo jumla ya vituo 13 vinatarajiwa kujengwa.

Aidha ametaja miradi iliyokamilika kuwa ni Mlimba mkoani Morogoro, Ludewa mkoani Njombe, Ruangwa mkoani Lindi, Ngara mkoani Kagera, Mlele mkoani Katavi pamoja na Kisaki mkoani Morogoro. Amesema, ujenzi unaendelea katika vituo vya Kyela mkoani Mbeya, Ngorongoro, Makete mkoani Njombe, Mbinga mkoani Ruvuma, Uvinza mkoani Kigoma, Lushoto mkoani Tanga pamoja na Kyerwa mkoani Kagera.

“Kazi zinajumuisha ujenzi wa vituo vipya, ukarabati wa studio za zamani na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa ambapo ruzuku iliyotumika ni shilingi bilioni 3.19 kwa mwaka wa fedha 2022/23. Maeneo yatakayonufaika ni pamoja na Chemba mkoani Dodoma, Chunya mkoani Mbeya na Kiteto mkoani Manyara na kwa gharama ya shilingi 1,350,000,000,” amesema Mtendaji Mkuu Mashiba.