UCSAF yaendelea kuboresha usikivu wa redio

  • 11 January, 2023
UCSAF yaendelea kuboresha usikivu wa redio

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Nape Moses Nnauye (Mb), amezindua kituo cha kurushia matangazo ya TBC FM na TBC Taifa katika Kata ya Inyonga wilaya ya Mlele mkoani Katavi, kituo kilichojengwa kwa ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF).

Mhe. Nnauye amesema, ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa malengo ya Serikali katika kuwafikia wananchi wote kwa kupanua usikivu wa radio ili kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha ameishukuru UCSAF kwa kufadhili ujenzi wa kituo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuimarisha usikivu wa radio katika maeneo mengine ya nchi yenye changamoto ya usikivu wa radio TBC FM na TBC Taifa.

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF Bi. Justina Mashiba amesema, ni jukumu la Mfuko huo kuhakikisha huduma za mawasiliano na usikivu wa radio zinawafikia wananchi wote popote pale walipo.