Mafanikio ya UCSAF katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru

  • 17 November, 2021
Mafanikio ya UCSAF katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru

Katika kipindi cha 60 ya Uhuru wa Taifa letu, Tanzania imeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ikiwemo sekta ya mawasiliano, kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ujumla. Urahisi huu wa Mawasiliano na ufikishaji wa Habari kwa wananchi umefikiwa baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi kwenye miundombinu ya mawasiliano.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.

Kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2019, Sekta ya Mawasiliano imekua kwa kasi ya asilimia 7.2 mwaka 2019. Ukuaji huu unathibitishwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano.

Kulingana na uchambuzi uliofanywa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) asilimia 66 ya ardhi ya Tanzania (Geographical Coverage) inafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani. Sekta hii huchangia katika uchumi moja kwa moja na kupitia sekta zingine zote kama nyenzo ya uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa utendaji kupitia teknolojia ya habari.

Dkt. Kijaji amesema Kabla ya Uhuru, Tanzania ilikuwa na mapungufu makubwa sana katika sekta ya Mawasiliano. Maeneo mengi ya Nchi hayakuwa na mawasiliano. Hivyo, Baada ya Uhuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Sekta mbalimbali zikiwemo Wizara, Taasisi za umma na binafsi inaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya mawasiliano ya simu, mifumo ya TEHAMA na utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya simu, redio na runinga, ujenzi wa minara ya mawasiliano na ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

Kutokana na changamoto hiyo, Mwaka 2009 Serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kuwezesha jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano maeneo ambayo hayana mawasiliano na hayana mvuto wa biashara ya mawasiliano hususan maeneo ya vijijini.

Amesema hadi sasa Tanzania ina jumla ya minara ya mawasiliano 12,902 ambapo minara 2,630 inatoa huduma ya 2G pekee na minara 9,579 inatoa huduma ya mawasiliano ya 2G, 3G au/na 4G. UCSAF imewezesha kujengwa kwa minara 1,068 kati ya minara tajwa hapo juu kwa kutumia ruzuku ya Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma. Hadi sasa takribani shilingi bilioni 161 zimetumika kujenga minara hiyo.

Ujenzi wa minara ya mawasiliano umefanyika kwenye kata 2,579 za Tanzania Bara kati ya kata 3,956 ambazo ni sawa na asilimia 65 na kwa upande wa Zanzibar, minara hiyo imejengwa kwenye kata 101 kati ya kata 110 ambazo ni sawa na asilimia 92. Mnara mmoja una uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano kutoka eneo mnara ulipo hadi eneo la umbali wa kilomita 11 kutegemea na jiografia ya eneo husika na aina ya masafa kwa kuwa huduma za mawasiliano kutoka katika mnara zinafika mbali zaidi kama eneo ni tambarare, halina misitu, miti mirefu, miinuko na milima.

Waziri Dkt. Kijaji amesema, Serikali katika azma yake ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ya uhakika na kwa gharama nafuu, Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, hivi karibuni imetangaza zabuni ya shilingi bilioni 37.7 za ujenzi wa minara 224 ya mawasiliano katika maeneo ya kimkakati na mipakani; kuhuisha teknolojia zilizokuwa zikitumika kwenye baadhi ya minara ambazo zilikuwa zina uwezo wa 2G kwenda kwenye teknolojia ya 3G na 4G; kufikisha huduma ya mawasiliano kwenye halmashauri kumi nchini ambazo ni halmashauri ya Mbogwe, Tanganyika, Kakonko, Malinyi, Mtwara Vijijini, Msala Vijijini, Pangani, Bariadi, Nzega na Kilindi.

Lengo likiwa kila mwananchi aweze kupata huduma za intaneti bila kujali yupo mjini au vijijini kwa sababu huduma ya intaneti ni huduma ya msingi kama ilivyo huduma ya mawasiliano ya simu ambayo kila mwananchi ana haki ya kupata huduma ya intaneti. Aidha, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatarajia kutangaza zabuni za huduma ya mawasiliano ya redio zenye jumla ya shilingi bilioni 1.5 kwa lengo la kuboresha mawasiliano ya redio ili kuongeza wigo wa wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati.