UCSAF Yatoa Sh. Bilioni 205.9 Kujenga Minara Vijijini

  • 16 February, 2023
UCSAF Yatoa Sh. Bilioni 205.9 Kujenga Minara Vijijini

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kutekeleza miradi ya mawasiliano ambapo imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 205.9 ikiwa ni mchango wa Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za mawasiliano vijijini.

 “UCSAF imeingia mikataba kufikisha huduma katika kata 1,242 zenye vijiji 3,654 na wakazi 15,130,250, imejenga minara 1,087 yenye vijiji 3,378 na wakazi 13,320,750. Aidha, utekelezaji unaendelea wa ujenzi wa minara 155 yenye vijiji 276 na wakazi 1,809,500 pamoja na mradi wa kimkakati wa Zanzibar unaohusisha minara 42, Shehia 38 ambapo ruzuku ya shiilingi bilioni 6.9 imetolewa,” ameeleza Mtendaji Mkuu Mashiba.

Kuhusu mradi wa kupeleka vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) shuleni Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa jumla ya shule 811 zimefikishiwa vifaa vya TEHAMA.

Amefafanua, “kwa wastani shule hupewa kompyuta tano, printa moja na projekta moja. Kwa mwaka wa fedha 2022/23, shule 150 zitafikishiwa vifaa vya TEHAMA ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 bajeti iliyotengwa ni shilingi 1,950,000,000."

Aidha,  kuhusu mradi wenye gharama ya shilingi 575,000,000, wa kupeleka vifaa maalum vya kujifunzia katika shule 16 zenye watoto wenye mahitaji maalum. Ametaja vifaa vitakavyotolewa kuwa ni TV, Nukta Nundu, Orbit reader (Machine za Kisasa), kompyuta mpakato, printa ya nukta nundu. 

Shule zitakazonufaika ni Shule ya Sekondari ya Mpwapwa (Mpwapwa-Dodoma), Shule ya Sekondari ya Mkolani (Mwanza), Shule ya Sekondari ya Kashaulili (Mpanda-Katavi), Shule ya Sekondari ya Morogoro (Morogoro), Shule ya Sekondari ya Shinyanga (Kishapu-Shinyanga), Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea), Shule ya Sekondari ya Kazima (Tabora) na Shule ya Sekondari ya Haile Selassie (Mjini Magharibi).