Habari

Walimu 650 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kunufaika na mafunzo ya TEHAMA.
  • 26 Oct, 2021
Walimu 650 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kunufaika na mafunzo ya TEHAMA.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. David Silinde amefanya ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyondaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT).

Akizungumza wakati wa Ufunguzi huo, Naibu Waziri Silinde amemshukuru Mwenyekiti wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF Prof. John Mkoma, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba  na watendaji wake kwa kuona umuhimu wa kufadhiri mafunzo haya kwa walimu 650 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ya TEHAMA kwa walimu nchini ni nyenzo muhimu katika kuwajengea uwezo wa kutumia na kuwapatia maarifa mbalimbali wanafunzi kwa urahisi, kwa kuwa yamezingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo imezungumzia matumizi ya TEHAMA katika ngazi zote za elimu. Sera hiyo imebainisha kuwa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 ulikwama kwa kiwango fulani kwa kuwa hakukuwa na mkazo katika  matumizi ya TEHAMA katika kufundisha na Kujifunzia.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala Pius Joseph amesema, mafunzo hayo ni muondelezo ya mafunzo ambayo yamekuwa yakifanyika kwa zaidi ya miaka mitano sasa, ambapo mwaka 2020 mafunzo kama haya yalifanyika kwa walimu 602.

Tamko Namba 3.3.5 Sera inaitaka Serikali kuweka utaratibu kusisitiza matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi zote. Sera inatambua kuwa Elimu inaweza kutolewa vizuri zaidi endapo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Rasilimali watu yenye ujuzi stahiki vitatumika. Hii pia ni katika kutambua mchango wa kujielimisha kwa njia mbalimbali zikiwemo elimu kwa njia ya Posta, elimu kwa njia ya Redio, Televisheni, matumizi ya Maktaba za Taifa na kisomo cha watu wazima.