UCSAF yajenga kituo cha miito ya dharura Zanzibar

  • 09 March, 2022
UCSAF yajenga kituo cha miito ya dharura Zanzibar

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Nape Nnauye amewataka watumishi watakaofanya kazi katika kituo cha miito ya dharura Zanzibar, (Zanzibar emergency call center) kuzingatia weredi katika utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na kutokuwa na majibu mabaya kwa wananchi watakaokuwa wakipiga simu kwa ajili ya kuhitaji huduma katika kituo hicho.

Mhe Nnauye ameyasema hayo wakati akikabidhi kituo hicho kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe, Rahma Kassim Ali. Kituo hicho kimejengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF) kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kutoa taarifa mbalimbali za dharura ikiwemo moto, afya, ajali na matukio mengine ya dharura.

Kwa upande wake Waziri Nnauye amesema, ujenzi wa kituo hicho pia unalenga kuipeleka Tanzania katika dunia ya kidigitali ambayo inataka upatikanaji rahisi wa huduma za mawasiliano na kwa muda wote.

Akipokea kituo hicho, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe, Rahma Kassim Ali amesema, Wizara itasimamia uendeshaji wa wake ikiwa ni pamoja na kuhakikikisha kuwa huduma zilizokusudiwa zinapatikana muda wote na kuahidi kuwa Serikali haitamvumilia mtendaji yoyote ambaye atakiuka taratibu za kazi katika katika kituo hicho.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Wizara ya  Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi ametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kutumia huduma ya kituo hicho kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali. Huku Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Bakari Amour, akiishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia UCSAF kwa kutekeleza mradi  huo mkubwa ambao pia ni wa kwanza kwa Zanzibar.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UCSAF, Profesa John Nkoma amesema, kuanzishwa kwa kituo hicho ni matokeo ya dhamira njema ya Serikali kupitia UCSAF katika kuhakikisha kuwa huduma ya mawasiliano inafikishwa kwa watanzania wote. Ametoa wito kwa wananchi kutumia kituo hicho wanapokuwa na mahitaji kweli na sio vinginevyo.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba, gharama za ujenzi wa kituo hicho ni shilingi milioni 200, ameongeza kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea jumla ya simu mia tano (500) kwa wakati mmoja. Kwa upande wa huduma zinazopatikana kituoni hapo, Mashiba amesema Mfuko unashirikiana na wataalam wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wizara ya Afya ambao ndio watakaokuwa wakipokea simu na kutoa huduma kwa wananchi.