Waziri Nape azitaka Taasisi zinazotoa vibali vya ujenzi wa minara kupunguza urasimu.

  • 24 January, 2022
Waziri Nape azitaka Taasisi zinazotoa vibali vya ujenzi wa minara kupunguza urasimu.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Nape Nnauye amezitaka Taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu kupunguza urasimu katika utoaji wa vibali hivyo ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Nnauye ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini  mkataba wa mradi wa kufikisha huduma za mawasiliano ya simu Visiwani Zanzibar ambao unatekelezwa na Kampuni ya simu ya mawasiliano Zanzibar (Zantel) kwa ruzuku ya shilingi bilioni 6.9 inayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Waziri amesema mchakato wa upatikanaji wa vibali kutoka mamlaka za Serikali kama vile mamlaka ya usafiri wa anga na Baraza la usimamizi wa mazingira umekuwa ukichukua muda mrefu kukamilika hali ambayo inasababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi mbalimbali ya mawasiliano ya simu nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhe. Rahma Kassim Ali ameipongeza Zantel kwa kushinda zabuni hiyo, huku akiwataka kutekeleza mradi huo kwa ubora unaotakiwa ili kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa watanzania wote hususani waishio visiwani Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema, kulingana na tathmini iliyofanywa na wizara hiyo, Tanzania inahitaji minara zaidi ya elfu mbili ili kumaliza kabisa tatizo la mawasiliano ya simu. Ambapo amesema hadi kufikia mwaka 2024 maeneo yote ya nchi yanatakiwa kuwa yamefikiwa na huduma za mawasiliano.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi Ndugu Amour Hamil, ameipongeza UCSAF kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mawasiliano ikiwemo ujenzi wa kituo cha miito ya dharura, mradi wa kuunganisha shule na mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA, ujenzi wa vituo kumi vya TEHAMA pamoja na mradi wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu. Ametaja mradi mwingine kuwa ni tiba mtandao ambapo Hospitali ya Abdula Mzee na Mnazi mmoja Zanzibar zitaunganishwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI) ili kuwezesha wananchi waishio pembezoni kupata huduma za madaktari bingwa.

Profesa John Nkoma ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UCSAF amemhakikisha Waziri Nnauye kuwa  Bodi  ya  mfuko, itakakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati kwa kuwa mawasiliano ni haki ya msingi ya kila mtanzania.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema, kwa mujibu wa mkataba  huo baina ya UCSAF na Zantel, mradi unatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa ambapo jumla ya minara 48 itajengwa, kila kata itajengewa mnara mmoja lakini baadhi ya kata zitakuwa na minara miwili kutokana na hali ya kijeografia katika eneo hilo.

Pemba ina Kata 12 na Unguja ina Kata 26 ambazo zitanufaika na mradi huo ambao utakapokamilika ziadi ya wananchi laki mbili watafikiwa na huduma ya mawasiliano.