Matokeo ya mafunzo ya TEHAMA kwa walimu

  • 08 November, 2021
Matokeo ya mafunzo ya TEHAMA kwa walimu

Benson Steven Mligo ni mmoja kati ya walimu walioshiriki mafunzo ya TEHAMA Kwa walimu wa shule za sekondari nchini yaliyokamilika wiki iliyopita katika vituo vitatu tofauti.

Baada ya kurejea katika kituo chake cha kazi, Shule ya Sekondari ya Magu Mkoani Mwanza, akaamua kutumia elimu aliyopata kurekebisha baadhi ya kompyuta ambazo walidhani zimeharibika.  Anasema

"Jambo la kwanza lilikuwa ni kuzifungua  kompyuta hizo mbili ili nijue zina tatizo gani. Hapo mwanzo kabla sijaja Dodoma kwenye mafunzo nilikuwa muoga sana wa kuzifungua kwa hofu ya kuziharibu; lakini baada tu ya mafunzo nikapata ujasiri wa kuzifungua ili nijue tatizo lilikuwa ni nini, kwa sababu kila kifaa nje ya kompyuta kilikuwa ni kizima. Nikapata wazo la kuazima blower machine kwa mafundi computer wa mtaani ili nizifanyie kwanza usafi. Baada ya usafi wa kutoa vumbi nikarudishia vifaa vyote kama vilivyokuwa. Mara paap! Kompyuta,....zikawaka. Nilifurahi sana. Kiukweli TROUBLESHOOTING & MAINTAINANCE ni muarobaini kwenye issue ndogondogo kama hizi" 

Tunampongeza mwalimu Mligo kwa kutumia vema mafunzo aliyoyapata. Tunashukuru pia wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma( UDOM) kwa kushirikiana na UCSAF katika kutoa mafunzo hayo.