Rais Mwinyi aipongeza UCSAF

  • 24 January, 2022
Rais Mwinyi aipongeza UCSAF

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapunduzi Dkt. Hussein Mwinyi amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye kwa kuteuliwa kushika washifa huo huku akimuahidi ushirikiano kutoka Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Wizara pamoja na taasisi zake.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Ikulu ya Zanzibar alipotembelewa na Waziri Nnauye akiwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe, Rahma Kassim Ali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amour Hamil, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Profesa John Nkoma, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba, mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza pamoja na watendaji wengine wa Wizara hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Nnauye alizungumzia pia utiaji saini wa makubaliano ya kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika shehia (kata) 38 visiwani Zanzibar ambayo yameingiwa na Serikali kupitia Mfuko wa mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kampuni ya mawasiliano Zanzibar (Zantel) ili kujenga minara ya simu 42 kwa lengo la kuboresha huduma ya mawasiliano visiwani humo.

Waziri Nnauye amemweleza Rais mwinyi kuwa makubaliano hayo  yanataka ujenzi wa minara yote 42 kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa, hata hivyo amesema urasimu katika mchakato wa upatikanaji wa vibali kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha miradi kama hiyo kukamilika kwa wakati.

Mhe, Rais Mwinyi  ameipongeza UCSAF kwa kutekeleza mradi huo pamoja na miradi mingine ya mawasiliano visiwani humo, na kisha kutoa agizo kwa mamlaka zote zinazohusika kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha mchakato wa upatikanaji wa vibali unakamilika ndani ya mwezi mmoja ili ujenzi  wa minara uanze na kumalizika kwa wakati kwa kuwa tatizo la mawasiliano ni kubwa na linahitaji ufumbuzi wa haraka.